Mgosi wa Sui

Mgosi wa Sui

Friday, February 20, 2015

Kuelekea Mechi na Mgambo Kocha Mtibwa atoa sababu lukuki


MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Bara ulikuwa ni mzuri sana kwa Mtibwa Sugar iliyokuwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo huku ikiwa na sare chache.
Mwendo wa Mtibwa Sugar ulikuwa unaivutia kila timu huku vigogo kama Yanga na Simba wakiendelea kusota kwa kuwa na matokeo yasiyokuwa na uhakika.

Mwishoni mwa mzunguko wa kwanza, hadi mwanzoni mwa mzunguko wa pili unaonekana kuwa shubiri kwa Mtibwa Sugar na sasa tayari imeishapoteza mechi tatu.
Mtibwa imepoteza mechi tatu, nyingi zaidi ya Yanga, Azam FC na Ruvu Shooting ambao mwanzo walionekana kama hawajakaa vizuri.
Kumekuwa na mengi yanayozungumzwa, kama timu hiyo imechoka kutokana na kucheza katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ilifika fainali na kufungwa na Simba.
Wengine wamekuwa wakisema mbinu za Kocha Mecky Maxime zimekuwa ni zilezile, sasa wengi wamejua namna ya kupambana nazo.
Championi Ijumaa liliona ni vizuri kumtafuta Maxime ili aweze kuelezea kutokana na anachokiona katika kikosi chake. Swali la kwanza lilikuwa ni hivi; Je, unafikiri umeishiwa mbinu na Mtibwa sasa itakwenda kwa mwendo wa kupapasa?
“Niseme kweli kuna matatizo, tunavyokwenda kumekuwa na mapungufu na kuna vitu vya kurejebisha.
“Suala la mbinu, kila mara tunabadili au kubaki vilevile kulingana na mechi. Naweza kusema kidogo kuna shida ya kisaikolojia baada ya wachezaji kutoka sare na kupoteza mfululizo inawaumiza, wanaona kama wamepotea au haiwezekani tena kurudi kama ilivyokuwa awali.
“Mimi na wenzangu wa benchi la ufundi, tunazungumza na wachezaji kila mara. Tunaamini hili litaisha,” anasema Maxime, beki wa zamani wa Mtibwa, Kilimanjaro Stars na Taifa Stars.
Mechi 7:
Tumecheza mechi sita ugenini, hatujawa na matokeo mazuri. Hili limewashangaza wengi kutokana na mwendo wetu katika mzunguko wa kwanza.
Sasa tunakwenda kucheza mechi ya saba, baada ya hapo tutarejea nyumbani na kupambana kuhakikisha tunashinda pia. Bado tutataka mechi inayofuata dhidi ya Mgambo licha ya kuwa ya ugenini, pia tushinde.
Ugumu:
Ligi ni ngumu sana kuliko watu wanavyoona, ndiyo maana unaona tofauti ya pointi kutoka timu moja na nyingine ni ndogo sana.
Ukifanikiwa kushinda mechi moja tu unakwenda mbali sana. Angalia Kagera Sugar, walipoteza mechi nafikiri tatu mfululizo, wakaamua kuhama Kirumba, Mwanza. Wamekwenda Shinyanga, wameshinda mechi mbili, sasa wako katika nafasi ya tatu.
Hii inaonyesha hakuna timu inayoshinda mechi tano mfululizo bila kupata sare au kufungwa. Huu ni udhibitisho wa ugumu wa ligi yetu.
Lawama:
Siwezi kuwa kocha wa tabia ya kulaumu wachezaji. Kweli kuna sehemu wanakosea, lakini lazima tujue makosa ni sehemu ya mchezo wa soka.
Ambacho nimekuwa nikifanya kwa kushirikiana na wenzangu wa benchi la ufundi ni kuwakumbusha majukumu yetu na kipi tunapaswa kufanya ili tuweze kurejea katika hali yetu.
Makosa:
Yanaweza kuwa mengi sana au kidogo lakini dawa ni kuyarekebisha. Najua baada ya hapo yatatokea tena, pia tutarekebisha na hii ni kawaida kabisa katika mchezo wa soka au maisha ya kawaida tu.
Kwenye safu ya ushambuliaji sisi tunapoteza nafasi nyingi za kufunga, mimi na wenzangu wa benchi la ufundi pia wachezaji, tunalifanyia kazi.
Mechi na Ndanda kule Mtwara tulitoka sare, lakini tulipoteza nafasi nyingi sana za kufunga, hadi ikapitiliza.
Angalia mechi na Yanga pale Taifa, tumefungwa bao 2-0. Kipindi cha kwanza sisi ndiyo tulipata nafasi tatu, hatukuzitumia kuumaliza mchezo.
Hapa lengo si kulaumu, badala yake kuonyesha namna gani tumekuwa tukikosea na tunaendelea kuyafanyia kazi matatizo hayo.
Haya pia yametokea kwenye safu za ulinzi katika mechi takribani zote tulizopata sare au kufungwa. Bado tunaendelea kuyafanyia kazi pia.
Imani yangu Mtibwa itarudi vizuri kabisa na kufanya vema. Inahitaji muda, inahitaji uvumilivu na ili tujirekebishe tuliamua tu kushughulikia wapi makosa yetu.
Utaona kila timu inataka kushinda nyumbani katika kila mechi wanayocheza. Kunaweza kuwa na juhudi za kawaida au zaidi, lakini kwa kifupi ligi ni ngumu na kila mmoja anatakiwa kulikubali hilo

No comments:

Post a Comment