Fainali ya kumsaka Bingwa
wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), inatarajiwa kufanyika kesho
kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuanzia majira ya saa 10 kamili jioni kwa
saa za Afrika Mashariki.
Awali mchezo huo wa
fainali ulikuwa umepangwa kufanyika kesho kwenye dimba la Uwanja wa Taifa,
lakini kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
nchini TTF imepelekea mchezo huo kuhamishiwa Chamazi.
Mchezo huo wa fainali
utaanza saa 10 kamili jioni, na utaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV
ili kuwapa nafasi wapenzi na wadau wa soka waliopo mbali na hasa mikoani kuweza
kushuhudia mchezo huo.
Bingwa wa Fainali ya Ligi
Daraja la Kwanza atazawadiwa Kombe pamoja na medali, huku mshindi wa pili
akipata kikombe na medali pia.
Viingilio vya mchezo huo
ni tsh.5,000 kwa jukwaa kuu na tsh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.
Wakati huo huo, Ligi Kuu
ya Vodacom inaendelea leo (Jumamosi) katika viwanja vitatu tofauti, Mgambo
Shooting watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
Ndanda FC ya Mtwara
watawakaribisha Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga katika
mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Ngwanda Sijaona.
Huku wakata miwa wa
Kagera Sugar wanaoutimia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakiwakaribisha
Maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mjini Morogoro timu ya Polisi.
Ligi hiyo ya Vodacom
itaendelea tena kesho jumapili katika viwanja vitatu tofauti, Uwanja wa Chamazi
wenyeji Azam FC wataikaribisha timu ya maafande wa Jeshi la Magereza nchini
Tanzania Prisons, mchezo utakaonza majira ya saa 2 kamili usiku.
No comments:
Post a Comment