
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema mdau mkubwa wa soka nchini, Damas Ndumbaro anajua sababu zinazokwamisha kusikilizwa kwa rufaa yake, lakini wakili huyo kitaaluma akaeleza “wasipoisikiliza itawatokea puani”.
Oktoba 13, mwaka huu, TFF kupitia kamati yake ya nidhamu ilimfungia daktari huyo wa sheria kujihusisha na shughuli za soka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa madai ya kwenda kinyume cha katiba ya shirikisho baada ya kuibuka mvutano kati yake na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Ndumbaro aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Klabu ya Simba na mjumbe wa Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB), alipinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya TFF kukata asilimia tano ya fedha za udhamini wa timu za Ligi Kuu, kitendo ambacho kilisababisha atupwe jela ya soka huku akikata rufaa ambayo hadi sasa haijasikilizwa na Kamati ya Rufaa ya shirikisho.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam juzi kuhusu kutosikilizwa kwa rufani hiyo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema: “Taratibu za kisheria ndizo zinakwamisha kusikilizwa kwa rufaa hiyo.”
Hata hivyo, katibu mkuu huyo wa zamani wa Yanga — Mwesigwa hakuwa tayari kueleza taratibu za kisheria zinazokwamisha kusikilizwa kwa rufani hiyo.
“Bahati nzuri Ndumbaro ni mwanasheria, anajua kwa nini hadi sasa rufani yake bado haijasikilizwa na Kamati ya Rufaa ya TFF,” alisema.
Alipotafutwa na NIPASHE jijini jana jioni, Ndumbaro alisema bado hajaelezwa kitu chochote na TFF kuhusu rufani yake aliyoiwasilisha katika ofisi za shirikisho hilo Oktoba 23 kupinga maamuzi ya kumfunga jela hiyo ya soka.
“Sijaelezwa chochote na TFF tangu nikate rufaa na hata hizo taratibu walizokwambia mimi hawajanieleza. Ninachosubiri ni kuitwa kwenda kusikiliza rufani yangu, na watasikiliza tu kwa sababu suala hilo lipo kikanuni na taratibu za shirikisho zinasema lazima rufani zisikilizwe.
“Wasipoisikiliza, itawatokea puani, lazima watasikiliza tu kabla sijachukua hatua zaidi. Taratibu zinasema ukishawasilisha rufani TFF na kulipa ada ya rufani (Sh. milioni moja), kinachofuata ni kuitisha kikao cha Kamati ya Rufaa ya TFF. Sasa wanahofia nini?” Ndumbaro alihoji.
“Tumejipanga kuhakikisha tunachukua hatua zaidi, siwezi kuziweka wazi kwa sasa maana nitakuwa ninavujisha mambo kabla ya wakati,” alisema.
Baadhi ya watendaji wa TFF (majina tunayahifadhi) waliozungumza na gazeti hili jijini wiki iliyopita walidai kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF wamekuwa wakikutana na Ndumbaro na kuomba achane na malumbano dhidi ya TFF.
Ndumbaro alikanusha madai hayo jana, kwa kusema: “Sijakutana na Malinzi wala mtu yeyote wa TFF kuzungumza kuhusu kumalizana kuhusu jambo hili nje ya taratibu za kisheria.”
Mtaaluma huyo wa sheria pia alikaririwa wiki tatu zilizopita akieleza kuwa mbali na kuziba mianya ya Sekretarieti ya TFF kuchota fedha za klabu kutoka TPLB kinyume cha taratibu, alionekana kuwa kikwazo kwa uongozi mpya wa shirikisho hilo akidaiwa kuwa ni miongoni mwa wadau wa soka wanaojipanga kuwania nafasi ya Rais wa TFF katika uchaguzi mkuu ujao wa shirikisho hilo.
No comments:
Post a Comment